Benedictus O. anasema kwamba aliweza kuhisi uhusiano na binti yake kabla ya kuzaliwa; ananieleza kuwa hata kabla ya mkewe kujua kuwa alikuwa mjamzito, yeye mwenyewe alijua kwa namna fulani na akajua kwamba mkewe atajifungua mtoto wa kike ambaye watamwita Amanda Meghan. Kuanzia mara ya kwanza alipomshika Amanda mikononi mwake, alihisi nguvu yake kwa kiasi kikubwa kupitia tabasamu aliompa;
Msichana huyu atakuwa wa kipekee duniani.
Na bila shaka, akiwa na umri wa miaka mitano, Amanda tayari ni mwangalifu sana na hutoa maoni yake bila woga, ni mtu ambaye ana shauku ya kuhusika katika kila kitu kinachotokea karibu naye iwe ni kusaidia kupika vyakula jikoni au kwenda kufanya kazi katika bustani, kujifunza kuhusu mimea na jinsi ya kuitunza, na pia kujaribu kwenda malishoni kuwachunga mbuzi na kondoo.
Hata hivyo, baada ya muda mfupi, mkondo ulibadilika walipoanza kutangamana na watu wengine, hasa alipotangamana na watoto wengine. Udhaifu mmoja wa Amanda ni kwamba alizaliwa akiwa na kivimbe kwenye sikio lake la kulia, hali aliyoionea aibu sana na hakuweza kutoka nyumbani bila kukificha kivimbe kile. Benedictus anakumbuka tukio hili kama hali iliyomsababishia uchungu mwingi yeye kama baba; siku zote alikusudia kukiondoa kile kivimbe, lakini hakutaka kufanya hivyo hadi wakati ambapo Amanda atakapokomaa kiasi cha kuweza kuelewa kilichokuwa kikiendelea, na pia kuhusika katika kuwasaidia kutafuta mtaalamu mwenye uzoefu wa kufanya hivyo. Kulikuwa pia na suala la kukusanya pesa za kufanya shughuli hiyo mbali na kumtafuta daktari, Benedictus anakiri kwamba hali ile ilikuwa sawa na “kupanda mlima mrefu”, ngumu kupita kiasi.
Baada ya kuondokewa na tatizo hilo, anasema sasa Amanda hatimaye anatumia kila nafasi kutangamana na watu na anapenda kwenda shuleni; mbali na masomo, anapenda kuwa shule pia inamfunza kuhusu kuwa mtu ambaye angependa kuwa. Babake anakumbuka bintiye alipokuja nyumbani kutoka shuleni siku yake ya kwanza na kumwambia kuwa mwalimu wake alikuwa amewahimiza wanafunzi wote wawape matunda na vyakula wale wanafunzi ambao hawakuwa na chakula; Amanda alikiri kuwa hakutaka kuwagawia kwa sababu hawakuwa na lolote la kumpa kama malipo. “La, mwanangu Amanda, hufai kufikiria hivyo.” alimwambia.
Kuwasaidia wengine ni tendo zuri sana kuliko matendo yote. Wape matunda, kalamu, kitabu, chochote ulichonacho ambacho wenzako wanahitaji. Usifikirie juu ya kile utakachopata kama fidia na utahisi furaha moyoni mwako.
Anasema kwamba siku iliyofuata, bintiye alifuata ushauri wake na akawagawia wenzake matunda aliyokuwa amemwandalia pamoja na chakula cha mchana; kufikia mwisho wa siku, alikuwa na marafiki watatu wapya; aidha, alitambua maana ya ndani ya ushauri ule na sasa anaishi kwa kufuata maadili haya. Anasema kwamba unahitaji tu kumwambia jambo mara moja naye atalitilia maanani.
Benedictus anasema kuwa wamekuwa wakisikilizana siku zote kama njia moja ya kuheshima. “Yeye hunifanya nitamani kutia bidii na kuwa mtu mwenye maadili mema kila siku.” anasema.
Na ninazungumza kwa niaba ya kina baba wote ulimwenguni sasa ninaposema kwamba tunahitaji kuhusika katika kuhakikisha binti zetu wanahisi vivyo hivyo. Kwamba wanaelimishwa, wanaheshimiwa, wanaungwa mkono na wanajua jinsi ya kujitegemea. Leo, mmoja kati ya wasichana kumi hujiua.
“Ni juu yetu sisi kuishi kama mifano ya kuwatia moyo. Nataka binti yangu awe jasiri kiasi cha kutosha katika kile anachofanya ili kuwapa wengine tumaini na kuwatia moyo wale wanaohitaji.”