Sio rahisi kuwa mwanamke

 

Mchungaji Ali ndiye wa kwanza kukiri kwamba sio rahisi kuwa mwanamke ambapo yeye yuko nchini Kenya. Baadhi ya wasichana katika kanisa lake hawawezi hata kununua sodo wanapokuwa na hedhi na wao hulazimika kukaa nyumbani na kutokwenda shuleni siku hizo; aidha, mambo ya kawaida ambayo yanaweza kuwafanya wawe na imani na kujiamini kama vile nguo zinazowafaa vizuri au kusukwa nywele zao ni adimu. Mapambano haya ya kila siku humtia maumivu anapoyashuhudia kwa kuwa anawachukulia wasichana hawa kama binti zake; kwake yeye kuwa baba si lazima iwe kibaolojia–inaweza pia kuwa kuwalea watu, kuwapa mwongozo, na kuwafundisha kile wanachohitaji kujua ili kujilinda. Hitaji hili la kujidhihirisha kama baba kwao ndilo lilimpelekea kubuni ufumbuzi wa matatizo ambao ulimfanya yeye na kanisa kuwasaidia wasichana hao.

 

Mbali na kuanzisha juhudi za kuchangisha pesa za kukidhi mahitaji yao ya kimsingi, pia aliandaa programu ya unasihi ambayo huwapa mafunzo ya kuelewa miili yao vizuri, hasa kuhusiana na jinsia yao, na umuhimu wa kujizuia kushiriki ngono hadi wanapoolewa ili wasiishie kupata watoto ambao hawawezi kuwalea. Programu hiyo pia inaangazia maana ya kuwa na uhusiano mzuri na mwanaume, kwani wasichana hao wengi hawajui baba zao, na maswala kama ulanguzi wa dawa za kulevya na uraibu, kwa bahati mbaya ni maswala yaliyoenea pote katika jamii kama ujauzito wa vijana ulivyoenea.

 

Mara wasichana hawa wanapokuwa wajawazito, huo ndio mwisho wao.

 

“Wanalazimika kuacha shule, kutelekeza ndoto zozote ambazo walikuwa nazo, na kuwageukia wazazi wao, ambao mara nyingi hawana uwezo wa kuwasaidia. Wengi wao huishia kuuza miili yao na wazazi wao kupuuza hayo. Wao huhisi kwamba hawana chaguo lingine la sivyo mtoto atakufa kwa njaa.” Nchi ya Kenya pia ilikuwa katika nafasi ya #2 kwa idadi ya wagonjwa wa UKIMWI, lakini kutokana na juhudi za kanisa hilo, anasema, imeshuka hadi nafasi ya #10 katika miaka ya hivi karibuni—jambo ambalo anatarajia litaendelea vivyo hivyo.

 

Mchungaji Ali anaona kuwa mahitaji ya binti zake ni tofauti sana na mahitaji ya mwanaume. Anasema kuwa anawake wanapotiwa moyo na msukumo, wanaweza kusimamia mambo mengi nyumbani na ndani ya mahusiano yao ya kibinafsi, jambo ambalo wanaume hawawezi. Anaongezea kwa kusema kuwa kwa bahati mbaya, utagundua kwamba unapokaribia wengi wao, wao huwa na maumivu makali ambayo hutokana na nyakati ambazo wema wao ulitumiwa vibaya.

 

Wanawake huhodhi mambo mengi zaidi ndani yao kuliko wanaume

 

“Msichana atabeba uzito huu wote ndani yake ambao hakuna mtu atakayeuona isipokuwa mtu atie juhudi ili kumkaribia na kuonyesha kuwa anaweza kuaminiwa. Na uponyaji wa maumivu haya ya ndani usipofanyika kwa njia ya uhusiano mzuri, makosa haya hujirudia mara nyingi na kusababisha madhara mengi zaidi.”

 

Ingawa janga la COVID-19 limesitisha juhudi zake kwa muda, anatumia wakati huo kubuni njia mpya za kuendeleza usaidizi wake mara wote watakapoweza kukusanyika tena. Mpango wake wa kwanza utakuwa kupanga karamu ya mlo wa jioni na kuwakaribisha watu wazima mashuhuri na wenye kutia motisha katika jamii ili washiriki hekima na mwongozo wao. Baada ya hotuba, kutakuwa na nafasi ya kila mtu kushiriki kile kilichomgusa katika hotuba hizo au ikiwa watapendelea, wataandika kwenye karatasi watakazopewa. “Wengi wao wana uzoefu sawa na ninaamini kuwa ushirikiano huu unaweza kuwafariji kwa namna fulani,” anaeleza, “Na hili likiwasaidia, nataka kukusanya uzoefu huu na kuandika kwenye kitabu–bila shaka kwa ruhusa yao na majina yao yakibadilishwa—ili wasichana wengine, popote walipo ulimwenguni, waweze kupata faraja kwa kukisoma ili kuwasaidia kuwakinga kutokana na hatari.”